UCHANGANUZI WA TAMTHILIA YA MFALME EDIPODE KAMA KAZI YA UHALISIAJABU
Abstract
Matini hii inahusu uhalisiajabu katika tamthilia ya Mfalme Edipode ya Sofokile. Katika matini hii nimechunguza uhalisiajabu katika kiwango cha wahusika na mandhari katika tamthilia hii nikiongozwa na nadharia ya Uhalisiajabu. Ili kufikia lengo langu, matini hii imegawanywa katika sehemu mbalimbali yaani; Utangulizi, mwili na hitimisho. Katika mwili wa matini hii, vipengele vya Uhalisiajabu vimechunguzwa na kubainishwa katika viwango vya wahusika na mandhari yenye matukio ya Uhalisiajabu. Vile vile,Matini hii imechanganua tamthilia ya Mfalme Edipode kwa kuegemea nadharia ya uhalisiajabu. Uhalisiajabu umeathiri kazi za kifasihi kwa upana na hujitokeza kwa namna mbalimbali. Suala la uhalisiajabu linafaa kuchunguzwa kwa sababu maisha yetu ya leo na hata jamii tunamoishi yametawaliwa na matendo ya kiajabu ambayo kwa kawaida hutuhangaisha na kutukanganya. Ukilinganisha na aina nyingine za nadharia zinazoyaendeleza na kuyaathiri maisha yetu, uhalisiajabu unajitokeza kwa kiasi
kikubwa ingawa huwa vigumu kwa baadhi ya binadamu kutambua kwa urahisi kuwa madhara yake huenda yakawa hatari zaidi. Aidha, kama kazi nyingine za fasihi zile, matendo yanayotendeka katika tamthilia ya Mfalme Edipode yanalenga kufunza na kuboresha jamii zetu hasa tukirejelea hatendo hayo kwa jicho la uangalifu. Vile vile, lugha iliyotumiwa katika tamthilia nzima inalingana sana na ya mazungumzo yetu ya kawaida kwa sababu zote hurejelea mitagusano ya kijamii ambapo wahusika hujibizana/huzungumzana moja kwa moja kuhusu mambo tofauti tofauti. Kwa kutumia nadharia ya uhalisiajabu kwa hiyo,matini hii, inadhihirisha kwamba baadhi ya mambo binadamu anayoyapitia huwa ya kutishia, ya kiajabu na ya kifantasia
zaidi na huenda yakaathiri mkondo wa maisha yake.