Mikinzano ya vizazi katika ukombozi wa mwanamke katika tamthilia ya "Mama Ee" na "Kilio cha Haki"
Mikinzano ya vizazi katika ukombozi wa mwanamke katika tamthilia ya "Mama Ee" na "Kilio cha Haki"
Date
2026
Authors
Irankunda, Allen
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
Makerere University
Abstract
Utafiti huu ulichunguza mikinzano ya vizazi katika ukombozi wa mwanamke kama ilivyojitokeza katika tamthilia za Mama Ee na Kilio cha Haki. Lengo kuu lilikuwa kuchunguza mikinzano ya vizazi katika mchakato wa ukombozi wa mwanamke. Utafiti uliongozwa na malengo matatu mahususi yaliyolenga kuchunguza namna mikinzano ya vizazi ilivyojitokeza katika tamthilia teule, kubainisha mitazamo ya wahusika wa kizazi cha zamani na kizazi kipya kuhusu ukombozi wa mwanamke, na kuchambua sababu zilizosababisha mikinzano hiyo. Utafiti ulitumia muundo wa kimaelezo na mbinu ya uchambuzi wa maudhui. Data za msingi zilipatikana kwa kusoma na kuchambua tamthilia za Mama Ee na Kilio cha Haki, huku data za upili zikikusanywa kutoka katika vitabu, makala za kitaaluma na tafiti tangulizi. Nadharia ya Mkinzano ilitumika kama mwongozo katika uchambuzi wa data. Matokeo ya utafiti yalibainisha kuwa mikinzano ya vizazi ilijitokeza kupitia tofauti za mitazamo kuhusu mila na desturi, elimu ya mwanamke, maamuzi ya familia, ndoa na upinzani dhidi ya mfumo dume. Kwa upande wa mitazamo, kizazi cha zamani kilielekea kutetea uhifadhi wa mila, utii na mamlaka ya mwanaume, ilhali kizazi kipya kilisisitiza elimu, usawa, haki, uhuru na ushiriki wa mwanamke katika maamuzi. Aidha, utafiti ulibaini kuwa tofauti za elimu, mila na desturi kandamizi, mfumo dume, mabadiliko ya kijamii na kiutamaduni, kuongezeka kwa mwamko wa wanawake kuhusu haki zao pamoja na athari za utandawazi zilichangia kusababisha mikinzano hiyo. Utafiti ulihitimisha kuwa mikinzano ya vizazi haikuwa chanzo cha migogoro pekee, bali pia ilikuwa kichocheo cha mabadiliko ya kijamii na ukombozi wa mwanamke. Kwa ujumla, tamthilia za Mama Ee na Kilio cha Haki zinaonesha nafasi ya fasihi ya Kiswahili katika kuakisi changamoto za kijamii, kuhoji mifumo kandamizi na kuibua masuala ya haki na usawa wa mwanamke.
Description
Tasnifu ya utafiti itakayowasilishwa katika idara ya Lugha za Kiafrika kwa ajili ya Kutosheleza Baadhi ya Masharti ya Kuhitimu Shahada ya Sanaa ya Chuo Kikuu cha Makerere
Keywords
Citation
Irankunda, A. (2026). Mikinzano ya vizazi katika ukombozi wa mwanamke katika tamthilia ya "Mama Ee" na "Kilio cha Haki"; Unpublished dissertation, Makerere University, Kampala.