KUCHANGANUA KILIO CHA HAKI KAMA TAMTHILIA YA KITANZIA
Abstract
Makala hii, imenuia kuchanganua udhihirikaji wa utanzia katika tamthilia iliyoandikwa na A. Mazrui. Lengo la utafiti huu ni kuchanganua Kilio cha Haki kama tamthilia ya kitanzia. Dhana ya utanzia katika makala hii ina maana ya, matendo au mazingira yanayozua jitimai, majonzi, masikitiko, majuto na maumivu ya mwili, roho au akili. Utanzia unajengwa na hali kama vile vifo,
ajali, vifungo, mabalaa, ulemavu, vilio, maradhi, njaa na mateso. Ila hakuna uchunguzi wa kutosha kuhusu matumizi ya utanzia katika kazi za fasihi ya Kiswahili. Hali hii imesababisha tatizo katika kuzielewa kazi mbalimbali za fasihi ya kiswahili. Utafiti huu ulifanyika mtandaoni, maktabani na kuyaduru mapitio ya maandishi mbalimbali kama vile tahakiki, makala na vitabu.
Utafiti ulitumia nadharia ya uhalisia wa kijamii. Uchambuzi wa data uliegemea nadharia hii katika maelezo.